Wakandarasi wazawa wathaminiwe

Aliyewahi kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, awamu ya tatu, Mh Benjamini William Mkapa amesema kuwa hakubaliani na mikataba ya Kimataifa ya kiuchumi ambayo inawanyima Watanzania haki ya kujiendeleza.
 
Mkapa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati anafungua mkutano wa makandarasi ulioandaliwa na Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB).
 
Akitoa mfano wa mikataba ya makandarasi, Makampuni kutoka Ulaya yanashinda zabuni mbalimbali nchini lakini ni nadra sana kwa makampuni ya Ujenzi ya kitanzania kufanya hivyo Ulaya.
 
“Wao wanaweza kuja hapa na wakashinda zabuni mbalimbali. Je, wewe ukienda Ulaya utashinda?,” alihoji Mh Mkapa.
 
“Wanasema kutakuwa na usawa sasa hapo ni usawa gani huo, napinga kabisa kwa sababu ni njia ya kuhakikisha…hahaha mmenielewa,” alisema.
 
Aidha Mh Mkapa alishauri Serikali kuwapa upendeleo maalumu wakandarasi wa ndani itakapoanza kulipa malimbikizo ya madeni wanayoidai.
 
Alisema hata kazi kubwa na nyingi za ujenzi wanapaswa kupewa wazalendo kwa kuwa kuna faida nyingi na fedha zinabaki nchini na kuleta maendeleo endelevu.
 
“Wakandarasi wazalendo wawezeshwe na wakamate soko la ujenzi kwa sababu wana uwezo ndiyo maana naona katika malipo ya malimbilizo ya madeni naomba Serikali iwape upendeleo maalumu,” alisema Mkapa.
 
Naye Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema Rais Jakaya Kikwete ameahidi kulipa madeni yote ya wakandarasi kabla ya kumaliza muda wake.
 
Alisema anatambua madai yote ya wakandarasi hivyo imeweka mipango katika bajeti ya mwaka huu kuhakikisha yanalipwa yote.
 
“Hakuna Serikali yoyote isiyodaiwa duniani, hakuna tajiri asiyedaiwa na Serikali ya Kikwete ni tajiri ndiyo maana inadaiwa,” alisema Dk. Magufuli.