Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejiment ya CRB wameendelea na ziara yao tarehe 19 Februari mwaka huu ambapo wametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo jijini Arusha unaojengwa na serikali kwa thamani ya shilingi bilioni 286.
Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Mhandisi Joseph Nyamhanga amemtaka Mkandarasi China Railway Construction Engineering Group Co. Ltd (CRCRG) kujumuisha Makandarasi wazawa katika ujenzi wa uwanja huo ili kuwajengea ujuzi na kuwa na uwezo.
“Ni vizuri kuwatumia Makandarasi wa ndani kwa kazi zinazofuata katika mradi huu ili kuwajengea ujuzi ili uwanja huu utakapokamilika wawe na uwezo wa kukarabati wakati wa matumizi”, alisema Mhandisi Nyamhanga.
Aidha mwakilishi wa Mkandarasi, Qs. Dennis Benito amesema kuwa wanafanya kazi usiku na mchana na hadi sasa wamefikia asilimia 25 ya utekelezaji na mpango wao ni kukamilisha mradi huo kabla ya muda wa mkataba ili watoe nafasi kwa wakaguzi wa michuano ya AFCON kukagua uwanja huo ili kutoa kibali cha fainali za AFCON 2027 yatakayofanyika katika uwanja huo.
Katika hatua nyingie Wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB walikagua mradi wa ujenzi wa jengo la matibabu ya moyo katika hosipitali ya rufaa ya kanda KCMC (Kilimanjaro Christian Medical Centre) wenye thamani ya shilingi bilioni 10 unaotekelezwa na mkandarasi Li Jun Development Construction Company Limited katika wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Baada ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Mhandisi Joseph Nyamhanga amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati ili uanze kuwahudumia wananchi.
Sambamba na hayo wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB wamefurahishwa na mkandarasi huyo kujumuisha wazawa kama sub-contractors waliopewa kandarasi mbali mbali na kuwataka makandarasi hao kuhakikisha wanatekeleza mradi kwa viwango na kwa wakati.
“Naomba nitoe wito kwa Makandarasi wa ndani walio kwenye mradi huu na Makandarasi wote wa ndani kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mikubwa hapa nchini ili kupata ujuzi na kujijengea uwezo wa makampuni yao ili waweze kutekeleza miradi mikubwa wenyewe," alisema Mhandisi Nyamhanga.
Aidha Mkadiriaji Majenzi Salvatori Mbwelwa amesema kuwa mradi huo ni wa miaka miwili na umeanza tangu Julai mwaka jana na mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 30 ya utekelezaji wake.
Pamoja na hayo Mhandisi David Mafuru kutoka hosipitali ya rufaa ya kanda KCMC ameshukuru ujio wa wajumbe wa bodi ya CRB katika mradi huo, na kueleza kuwa utaongeza kasi ya mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati ili kusogeza huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi wa kanda ya kaskazini ambao husafiri kwenda jijini Dar es Salaam kufata huduma hiyo.
Aidha wajumbe wa Bodi hiyo wametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la mahakama ya Afrika ya binadamu na watu katika eneo la Lakilaki Wilayani Arumeru Mkoani Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 62 unaotekelezwa na mkandarasi CRJE (EAST AFRICA) LIMITED.
Mradi mwingine uliotembelewa na Bodi hiyo ni pamoja na ujenzi wa jengo la taaluma katika chuo cha ushirika Moshi unaotekelezwa na Mkandarasi wa ndani TIL Constrctuction Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 3.2 na ujenzi wake umefikia asilimia 41.
Photo by:Admin, 2025-03-26 05:51:22 |
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi CRB Mhandisi Joseph Nyamhanga, amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi wa usambazaji wa umeme vijijini (REA) mkoa wa Manyara katika Wilaya ya Babati, Simanjiro na Kiteto, na kampuni ya China Railway Construction Electrification Bereau Group Company Limited (CRCEBG) kukamilisha mradi huo kwa wakati ili wananchi wapate huduma ya umeme.
Amesema hayo tarehe 18 Februari mwaka huu katika ziara ya Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya CRB inayofanywa katika mikoa minne ya kanda ya kaskazini ambayo ni Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa lengo la kukagua kazi za Makandarasi.
Mhandisi Nyamhanga amesema kuwa hatua ya serikali kusambaza umeme katika kila kitongoji nchini imelenga kuhakikisha kila mwananchi anafikiwa na huduma ya umeme kwa gharama nafuu.
Aidha msimamizi wa mradi Mhandisi Michael Masimbani amesema mradi huo umelenga kufikisha huduma ya nishati ya umeme katika kata 139 ambao thamani yake ni zaidi ya shilingi bilioni 21na miongoni mwa wanufaika ni pamoja na kitongoji cha Maisaka ambapo tayari nguzo zimeshasimikwa na nyaya zimeshavutwa na kwamba kilichosalia sasa ni ufungaji wa transfoma.
Aidha ujumbe huo wa Bodi na Menejimenti CRB umetembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa makumbusho ya Hifadhi ya Ngorongoro wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 23 unaotekelezwa na Mkandarasi China Railway 25 Group Ltd katika Wilaya ya Ngorongoro.
Akitoa taarifa kwa wajumbe hao wa Bodi ya CRB Mjeolojia Ramadhan Khatibu kutoka Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro amesema makumbusho hayo yanatarajiwa kukamilika mwezi mei mwaka huu ambapo itaongeza idadi ya watalii watakao tembelea katika hifadhi hiyo.
Sambamba na hayo Bodi hiyo imetembelea mradi wa upanuzi wa maji wa kilometa 48 unaotoka tenki la maji la Ngorbob jijini Arusha unaotekelezwa na Mkandarasi Jandu Pumblers Ltd katika eneo la Nanja wilaya ya Monduli ambao umelenga kutatua changamoto ya maji kwa wakazi wa wilaya hiyo na vijiji vya jirani.
Pamoja na hayo Mwenyekiti wa Bodi ya CRB Mhandisi Nyamhanga amemtaka Mkandarasi Jandu Plumbers kuhakikisha anakamilisha mradi huo kwa kwa ubora unaotakiwa kwa kuzingatia gharama halisi kwa mujibu wa mikataba yao ili kutimiza azma ya Serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kwa wakati.
Photo by:Admin, 2025-03-26 05:48:21 |
Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imesema inaanza operesheni maalum ya kukagua miradi mikubwa inayotekelezwa na Makandarasi kutoka nje ya nchi, kutokana na miradi mingi kutekelezwa chini ya viwango.
Aidha imebaini hayo kufuatia ziara mbalimbali za Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa katika miradi mbalimbali ikiwemo barabara ambayo imeonekana kuwa na changamoto kubwa.
Akizungumza leo jijini Arusha, katika ufunguzi wa mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa Makandarasi,Msajili wa CRB, Rhoben Nkori, alisema Bodi hiyo imeamua kufanya operesheni hiyo maalum kuanzia mwezi Mei hadi katikati ya mwezi Juni mwaka huu.
Aliwataka Makandarasi wote kutambua kuwa operesheni hiyo maalum itafanyika hadi mwezi Juni, 2024 ili kujiridhisha Makandarasi wote walioingia mkataba na serikali kama wanafanya kwa mujibu wa mikataba waliyoingia na sheria, kinyume na hapo hatua zitachukuliwa.
“Bodi iemamua kufanya operesheni maalum ya kutembelea miradi na kukagua miradi yote mikubwa inayofanywa na wakandarasi wa nje kwasababu miradi mingi mikubwa inafanywa na wakandarasi wa nje,”alisema.
Photo by:Admin, 2024-05-16 06:26:32 |