Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, ameagiza Wizara kupitia Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), kuhakikisha wanakuja na mikakati ya kuwawezesha Makandarasi Wazawa kushirki katika Utekelezaji wa miradi ya Sekta ya Ujenzi nchini ili kuleta tija kwa Makandarasi hao na Taifa kwa ujumla.
Ameyasema hayo Septemba 26, 2023 jijini Dodoma, wakati alipokutana na kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu ya Taasisi za Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC).
Bashungwa ameagiza Wizara kukaa na kusikiliza changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi pamoja na kuandaa mikakati itakayosaidia makandarasi hao kutekeleza miradi mingi hasa ya kimkakati itakayoweza kuinua mitaji yao.
“Linapokuja suala la ‘Local content’ yaani fursa za kiuchumi kwa watanzania, Mheshimiwa Rais kiu yake ni kuona ushiriki wa Makandarasi wazawa kwenye maendeleo ya Sekta ya Ujenzi unaongezeka”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameeleza kuwa Takwimu zilizopo zinaonyesha kuwa idadi ya Makandarasi waliosajiliwa na Bodi ni 14,550 ambapo kati ya hao 550 ni Makandarasi wa nje na 14,000 ni Makandarasi wazawa lakini katika utekelezaji wa miradi Makandarasi Wazawa wanapata asilimia 46 na Makandarasi wa nje wanapata asilimia 54.
Aidha, Bashungwa ameishukuru Serikali kupitia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maboresho aliyoayaagiza katika sheria ya manunuzi kwa miradi yenye gharama ya kutoka Bilioni 10 hadi 50 kupewa kipaumbele kutekelezwa na makandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo.
Kuhusu madeni kwa Makandarasi, Waziri Bashungwa amesema kuwa kupitia Wizara ya Fedha, Serikali imeshaweka utaratibu wa kulipa madeni hayo ambapo hivi sasa kila mwezi kuanzia mwezi wa nane kiasi cha Bilioni 70 kinatengwa ambapo Bilioni 50 zinalipa madeni ya makandarasi wa ndani na Bilioni 20 ni kwa ajili ya kulipa Makandarasi wa nje.
Bashungwa pia ameziagiza Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi kuhakikisha zinabuni mikakati ya kutangaza mafanikio na kazi zao kwa umma ili kuleta tija katika Taasisi hizo na Taifa kwa ujumla.
Kadhalika, Bashungwa ameziagiza Taasisi hizo kusimamia wataalamu wao ili kuhakikisha wanatoa huduma sahihi na kwa wakati kwa umma na kuhakikisha wanachukua hatua kwa wale ambao watakiuka maadili ya kazi zao.
Photo by:Admin, 2023-09-27 08:34:12 |