BODI ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imewataka makandarasi kuacha woga kwenye kudai haki zao pale mikataba yao inapokiukwa kwa kuhofia kuharibu uhusiano na wateja wao.
Wito huo umetolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Consolatha Ngimbwa, wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kuhusu usimamizi wa mikataba kwa Makandarasi wazalendo.
Amewaasa watumie ujizi watakaoupata badala ya kuishia kwenye vitabu tu kwani uzoefu unaonyesha kwamba wapo Makandarasi ambao pamoja na kuwa na ujuzi, bado wanashindwa kusimamia haki zao eti kwa kuogopa kuharibu uhusiano na waajiri.
“Msifanye hivyo kwa sababu katika mikataba Mkandarasi ana wajibu na haki zake na mwajiri vivyo hivyo. Hebu jiulize kwa nini Mkandarasi akikiuka makubaliano mwajiri hasiti kumchukulia hatua? Mbona Mwajiri haogopi kuharibu uhusiano,” amesema.
Kadhalika, amewataka makandarasi wazalendo kutokurupuka wakati wa kusoma mikataba ya ujenzi ili kuepuka hasara wanayoweza kupata na wakati mwingine kukimbia kazi wanazopewa.
Amesema usimamizi mzuri wa mikataba ni ujuzi wa muhimu na wa lazima kwa Makandarasi kwa sababu kimsingi kazi ya ukandarasi ni mikataba na kwamba nyakati zote, mkandarasi anashughulika na mikataba.
SOURCE: MICHUZI BLOG 02/12/2021.
Photo by:Admin, 2022-01-01 08:30:51 |
MAKANDARASI wametakiwa kuacha kuomba zabuni kwa gharama za chini, ili kuwavutia watoaji wa kazi, kwa kuwa uzoefu unaonyesha wamekuwa wakishindwa kuzikamilisha na wengine kukimbia baada ya kuzipata.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Morogoro na Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Mhandisi Consolata Ngimbwa wakati akifungua mafunzo ya siku tatu kwa makandarasi wazalendo.
Alisema baadhi ya makandarasi wamekuwa wakijaza hela ndogo kama mbinu ya kushinda zabuni lakini wanapopata kazi hizo wanashindwa kuzikamilisha kwa wakati na wengine kushindwa kuzikamilisha kabisa.
“Jazeni zabuni vizuri tena kwa uhalisia msijaze tu ilimpate zabuni lakini mwishowe zinawashinda, hapa katikati tuliyumba sana baada ya serikali kuanza kufanyakazi zake kwa kutumia utaratibu wa force account sasa tumeanza kupata kazi za serikali tusifanye makosa, tuzifanye kwa weledi mkubwa,” alisema Ngimbwa.
Alisema CRB iliamua kuanza kutoa mafunzo hayo kwa makandarasi baada ya lawama nyingi kwamba makandarasi hao wamekuwa wakiweka bei ambazo hazina uhalisia.
Mhandisi Ngimbwa aliwasisitiza pia kufanyakazi kwa ubia na makandarasi wenzao na wanaposhindwa kujua namna ya kuzifanya wafike ofisi za bodi hiyo au kwa wataalamu kwaajili ya kuelekezwa namna ya kufanyakazi za aina hiyo.
“Wengi tunaingia kwenye kazi za ubia lakini tunashindwa sijui kwasababu hatuzijui au, uzuri wa kazi hizi ni kwamba mnaunganisha nguvu na kufikia vigezo vinavyohitajika na kama mkishindwa njooni CRB mtaelekezwa,” alisema.
SOURCE: "Nipashe Alhamisi Agosti 12,2021"
Photo by:Admin, 2021-08-17 12:30:10 |
MAKANDARASI nchini wameelezwa kuwa matumizi ya mfumo wa manunuzi ya umma kielekroniki (TANePS) ni ya lazima kwao hivyo wanapaswa kuufahamu vyema na kuutumia kwaajili ya kuwasilisha zabuni zao mapema.
Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB),Qs Joseph Tango, wakati wa mafunzo ya namna ya kutumia mfumo huo na wajibu wa mkandarasi.
Tango alisema ni muhimu kwa makandarasi kufanya maandalizi ya zabuni mapema na kuziwasilisha kwa njia ya mfumo huo kama ni mradi wa serikali kwani tabia ya kufanya kwa mtindo wa zimamoto hauwezi kuleta matokeo mazuri.
“Kwenu nyinyi ujuzi wa kutumia mfumo huu wa kielektroniki ni lazima kwasababu mwajiri mkubwa wa mkandarasi ni serikali na kwa sasa huwezi kushiriki zabuni ya kazi za serikali bila kupitia mfumo huu.” alisema
“Na mjenge kawaida ya kufanya mapema kwani mfumo huu ni wa kielektroniki na chochote kinaweza kutokea na kukufanya uchelewe kuwasilisha zabuni kwa mfano hitilafu ya umeme mahali ulipo au udhaifu wa mtandao wa intaneti haya yote yatakukwamisha.” Alisema.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Qs. Joseph Tango akifunga mafunzo ya siku tatu kuhusu wajibu wa makandarasi na namna ya kujaza zabuni kielektroniki yaliyoendeshwa na bodi hiyo mkoani Morogoro kwa siku tatu na kumalizika siku ya Ijumaa.
SOURCE: "HABARILEO JUMATATU AGOSTI 16,2021","Nipashe Jumatatu Agosti 16,2021"
Photo by:Admin, 2021-08-17 11:39:52 |