Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ametoa siku 30 na kumtaka Mkandarasi Kampuni ya CHICO anayetekeleza ujenzi wa upanuzi wa barabara ya Nsalaga - Ifisi (km 29) kwa njia nne, jijini Mbeya kuongeza kasi ya ujenzi wa mradi huo ili uweze kukamilika na kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo.
Aidha, Waziri Ulega amemuagiza Mkandarasi huyo kufanya kazi usiku na mchana, kuongeza vifaa pamoja wafanyakazi ili kufanikisha mradi huo ukamilike haraka iwezekanavyo.
Ulega ametoa maelekezo hayo jijini Mbeya wakati alipokuwa akikagua maendeleo ya mradi huo na kutoridhishwa na hatua za utekelezaji wake ambao hadi sasa umefikia asilimia 25.
Ulega ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari imeshatoa malipo ya Shilingi Bilioni 35 kwa Mkandarasi huyo na matarajio yake ni kuona kupitia fedha hizo angalau kilometa kadhaa za lami zimekamilishwa kujengwa katika barabara hiyo.
“Serikali imeshatoa Bilioni 35 kwa ajili ya ujenzi wa barabara hii kutoka Nsalaga hadi Ifisi, na fedha hizi Mkandarasi hajazifanyia kazi ipasavyo, Sasa basi Nimemuagiza Mkandarasi afanye kazi usiku na mchana na kuona mabadiliko ya haraka katika mradi huu”, amesisitiza Ulega.
Pia, ametoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi kwa ukaribu ili hadi kufikia mwanzoni mwa Mwezi Juni mwaka huu Mkandarasi awe amekamilisha kilometa 10 za lami katika barabara hiyo na kuahidi kurudi tena kwa ajili ya kukagua maendeleo hayo.
Ulega amemuelekeza Meneja huyo wa TANROADS kuhakikisha ujenzi wa barabara hiyo unaenda sambamba na ufungaji wa taa za barabarani ili kuupendezesha mji wa Mbeya na kuimarisha masuala ya ulinzi na usalama wa wananchi wanaotumia barabara hiyo katika shughuli zao za kiuchumi za kila siku.
Vilevile, Ulega amepokea Ombi la Mbunge wa Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson la ujenzi wa kilometa tano za lami zinazoingia katika mitaa ya iiji la Mbeya na kuahidi kulifanyia kazi.
Kadhalika, Ulega amemuagiza Meneja wa TANROADS mkoa wa Mbeya kumsimamia Mkandarasi katika kuhakikisha kazi ndogondogo zinazofanywa na Mkandarasi zinatolewa kwa vijana wa Mkoa wa Mbeya ili kutoa fursa za ajira na vijana hao waweze kunufaika na matunda ya mradi.
kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini na Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameeleza kuwa wananchi wa Mbeya wamekuwa wakisubiri kwa hamu upanuzi wa barabara hiyo kukamilika ili kutatua changamoto za msongamano wa magari jijini humo.
Dkt. Tulia ameiomba Wizara ya Ujenzi kufanyia kazi mapendekezo yaliyoombwa katika barabara hiyo ya kuongezwa kwa barabara kilometa 3.5 kuanzia Ifisi hadi Songwe Airport na kilometa 5 kuanzia Nsalaga kuelekea Mlima Nyoka katika Bajeti mpya ya mwaka 2025/26 ili wananchi wa Mbeya kuendelea kunufaika na ujenzi wa mtandao wa barabara jijini humo.
Naye, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mbeya, Eng. Matari Masige ameeleza kuwa Mkandarasi anaendelea na ujenzi wa matabaka ya udongo G3, G7 na G15, ujenzi wa makalvati madogo na makubwa pamoja na ujenzi wa daraja la Nzovwe katika barabara hiyo.
Photo by:Admin, 2025-04-23 06:48:31 |
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi CRB Mhandisi Joseph Nyamhanga, amezitaka Taasisi za Umma kuzingatia sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 na kanuni zake za mwaka 2024 ambazo zinaelekeza kuwa mikataba ya miradi ambayo haizidi shilingi Bilion 50 inatakiwa itekelezwe na Makandarasi wazawa.
Amesema hayo tarehe 20 Februari mwaka huu katika mwendelezo wa ziara ya Bodi ya Wakurungenzi na Menejimenti ya CRB inayofanywa katika mikoa minne ya Kanda ya kaskazini ambayo ni Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kwa lengo la kukagua utendaji kazi wa Makandarasi na utekelezaji wa Miradi.
"Sisi kama Bodi tunaendelea kushauri Taasisi za Umma ziendelee kuzingatia sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2023 pamoja na kanuni zake za mwaka 2024 kutoa kandarasi ndogo ambazo hazizidi shilingi bilioni 50 kwa Makandarasi wa ndani na hii itakua namna nzuri ya kuwajengea uwezo na kuhakikisha kwamba fedha hizi zinabaki hapa nchini”, alisema Mhandisi Nyamhanaga.
Sambamba na hayo Mhandisi Joseph Nyamhanga, ametumia fursa hiyo kuzitaka kampuni za kigeni zinazojenga miradi nchini kutoa kandarasi ndogo (sub-contractors) zenye thamani kubwa ya fedha kwa Makandarasi wazawa ili miradi hiyo iwajengee uwezo.
Mhandisi Nyamhanga aliyasema hayo wakati wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB walipotembelea mradi wa usambazaji umeme vijijini (REA) katika mkoa wa Kilimanjaro wenye thamani ya shilingi bilioni 18.4 wenye urefu wa kilometa 270 unaotekelezwa na Mkandarasi Ceylex Engineering (PVT) Ltd kutoka SiriLanka.
Akitoa taarifa kwa wajumbe wa Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya CRB, Meneja wa mradi Mhandisi Sakina Mohammed amesema kuwa mradi huo wa usambazaji wa umeme vijijini (REA) ni wa miaka miwili na utasambazwa katika vitongozi 135 vya mkoa wa Kilimanjaro na mpaka sasa umefikia asilimia 11.6 ya utekelezaji wake.
Katika hatua nyingine Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejimenti ya CRB, walitembelea mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi wenye thamani ya shilingi trilioni 1.4 unaotekelezwa na Mkandarasi China Petroleum Pipeline Engineering Co. Ltd (CPP) katika kijiji cha Misino, Wilaya ya Handeni Mkoani Tanga na kuridhishwa namna mradi huu unavyotekelezwa.
Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa mradi huo Mwenyekiti wa Bodi ya CRB Joseph Nyamhanga amempongeza Mkandarasi huyo kwa kuajiri watanzania kwa zaidi ya asilimia 70 pamoja na kutoa fursa ya kandarasi ndogo (Sub – Contractors) kwa Makandarasi wazawa, ambapo pia amewataka Makandarsi hao kukamilisha mradi kwa viwango na kwa wakati.
“Ni jambo zuri kutoa ajira kwa wazawa, lakini pia nimefurahi ametoa kandarasi ndogo kwa Makandarasi watatu kwa kipande kinacho anzia mkoa wa Singida hadi hapa Tanga”. Amesema Nyamhanga.
Akitoa taarifa ya mradi huo Willhel kiria ambaye ni meneja wa mazingira katika mradi huo,amesema mradi huo pia unazingatia uhifadhi wa mazingira kwani utekelezaji wake hauharibu miundombinu iliyopo.
“Hapa katika kivuko cha barabara hii tunatoboa chini kwa urefu wa mita 48 ili tuweze kupitisha bomba, tukimaliza hapa tunahamia katika kivuko kingine”. amesema Kiria .
Wajumbe hao wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB, pia wametembelea kambi namba 16 ya Mkandarasi China Petroleum Pipeline Engineering (CPP) iliyopo katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga ambapo wameshuhudia maandalizi ya awali ya kambi ikiwa na utayari wa kuanza ulazaji wa bomba hilo la mafuta ghafi utakao anzia Kabaale - Hoima nchini Uganda na kuishia Chongoleani mkoani Tanga nchini Tanzania.
Wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB wanaendelea na ziara ya kukagua miradi mbalimbali katika mikoa ya kanda ya kaskazini,ambapo wanatarajia kukamilisha Ziara yao jijini Tanga.
Photo by:Admin, 2025-03-26 05:54:08 |
Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi pamoja na Menejiment ya CRB wameendelea na ziara yao tarehe 19 Februari mwaka huu ambapo wametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo jijini Arusha unaojengwa na serikali kwa thamani ya shilingi bilioni 286.
Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Mhandisi Joseph Nyamhanga amemtaka Mkandarasi China Railway Construction Engineering Group Co. Ltd (CRCRG) kujumuisha Makandarasi wazawa katika ujenzi wa uwanja huo ili kuwajengea ujuzi na kuwa na uwezo.
“Ni vizuri kuwatumia Makandarasi wa ndani kwa kazi zinazofuata katika mradi huu ili kuwajengea ujuzi ili uwanja huu utakapokamilika wawe na uwezo wa kukarabati wakati wa matumizi”, alisema Mhandisi Nyamhanga.
Aidha mwakilishi wa Mkandarasi, Qs. Dennis Benito amesema kuwa wanafanya kazi usiku na mchana na hadi sasa wamefikia asilimia 25 ya utekelezaji na mpango wao ni kukamilisha mradi huo kabla ya muda wa mkataba ili watoe nafasi kwa wakaguzi wa michuano ya AFCON kukagua uwanja huo ili kutoa kibali cha fainali za AFCON 2027 yatakayofanyika katika uwanja huo.
Katika hatua nyingie Wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB walikagua mradi wa ujenzi wa jengo la matibabu ya moyo katika hosipitali ya rufaa ya kanda KCMC (Kilimanjaro Christian Medical Centre) wenye thamani ya shilingi bilioni 10 unaotekelezwa na mkandarasi Li Jun Development Construction Company Limited katika wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro.
Baada ya ukaguzi wa mradi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya CRB, Mhandisi Joseph Nyamhanga amemtaka mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati ili uanze kuwahudumia wananchi.
Sambamba na hayo wajumbe wa Bodi pamoja na Menejimenti ya CRB wamefurahishwa na mkandarasi huyo kujumuisha wazawa kama sub-contractors waliopewa kandarasi mbali mbali na kuwataka makandarasi hao kuhakikisha wanatekeleza mradi kwa viwango na kwa wakati.
“Naomba nitoe wito kwa Makandarasi wa ndani walio kwenye mradi huu na Makandarasi wote wa ndani kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa miradi mikubwa hapa nchini ili kupata ujuzi na kujijengea uwezo wa makampuni yao ili waweze kutekeleza miradi mikubwa wenyewe," alisema Mhandisi Nyamhanga.
Aidha Mkadiriaji Majenzi Salvatori Mbwelwa amesema kuwa mradi huo ni wa miaka miwili na umeanza tangu Julai mwaka jana na mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 30 ya utekelezaji wake.
Pamoja na hayo Mhandisi David Mafuru kutoka hosipitali ya rufaa ya kanda KCMC ameshukuru ujio wa wajumbe wa bodi ya CRB katika mradi huo, na kueleza kuwa utaongeza kasi ya mkandarasi kukamilisha mradi huo kwa wakati ili kusogeza huduma ya matibabu ya moyo kwa wananchi wa kanda ya kaskazini ambao husafiri kwenda jijini Dar es Salaam kufata huduma hiyo.
Aidha wajumbe wa Bodi hiyo wametembelea na kukagua mradi wa ujenzi wa jengo la mahakama ya Afrika ya binadamu na watu katika eneo la Lakilaki Wilayani Arumeru Mkoani Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 62 unaotekelezwa na mkandarasi CRJE (EAST AFRICA) LIMITED.
Mradi mwingine uliotembelewa na Bodi hiyo ni pamoja na ujenzi wa jengo la taaluma katika chuo cha ushirika Moshi unaotekelezwa na Mkandarasi wa ndani TIL Constrctuction Ltd kwa gharama ya shilingi bilioni 3.2 na ujenzi wake umefikia asilimia 41.
Photo by:Admin, 2025-03-26 05:51:22 |